Zitto na Demokrasia

Zitto na Demokrasia

MKATABA WA GESI WA STATOIL NA TANZANIA

leave a comment »

MKATABA WA GESI WA STATOIL NA TANZANIA

Swali kwa TPDC: Kwanini Makubaliano ni tofauti na Mkataba Elekezi (Model PSA)?

Baada ya kuvuja kwa Mkataba wa kutafuta na kuzalisha Gesi Asilia (PSA) kati ya Serikali kupitia TPDC na Kampuni ya Norway ya StatOil na baada ya baadhi ya wachambuzi kuhoji kuhusu mkataba huo, Shirika la TPDC limetoa maelezo yake. Sio mara moja, sasa ni mara ya tatu. Kimsingi TPDC wanasema wachambuzi waliochambua nyongeza hiyo ya Mkataba hawana uelewa wa mambo haya na wanaleta siasa. Nadhani ni muhimu TPDC wakajikita katika kueleza kwa lugha ambayo wananchi wa kawaida wataelewa badala ya kusingizia uelewa wa watu katika masuala haya. Wizara ya Nishati na Madini haina uelewa wa pekee wa masuala ya Mafuta na Gesi kama wanavyotaka umma uamini. Kuna watanzania wengi tu wenye kufuatilia mambo haya na wenye uwezo mpana hasa katika masuala ya kodi katika tasnia hii. Ni wajibu wa TPDC kutoa maelezo yasiyo changanya wananchi na bora zaidi waweke mikataba hii ya Gesi na Mafuta wazi. Maelezo yaliyotolewa na TPDC mpaka sasa hayaeleweki na yana lengo la kuwachanganya wananchi kama sio kuwaongopea.

Swali la Msingi

Serikali kupitia “Model PSA” imeweka viwango vya mgawanyo wa mapato kati ya Mwekezaji na nchi. Viwango hivi ni vya mgawo wa mafuta au gesi asilia yanayozalishwa kwa siku. Mkataba huu elekezi upo kwenye tovuti ya Shirika la TPDC na ndio mwongozo wa majadiliano kwa mikataba yote. Kwa mujibu wa Mkataba huu elekezi uzalishaji wa gesi asilia unapokuwa wa chini kabisa (0 –249.999 MMscf kwa siku) mgawo kati ya Tanzania na Mwekezaji unakuwa ni nusu kwa nusu (50 – 50 ) baada ya mwekezaji kuondoa gharama zake zote za uzalishaji.

Iwapo uzalishaji umefikia hali ya juu kabisa ( 1500 MMscf na zaidi) mgawo wa Tanzania unakuwa asilimia 80 na Mwekezaji asilimia 20. Mwekezaji anaruhusiwa kuchukua mpaka asilimia 70 ya Gesi iliyozalishwa kufidia gharama za uzalishaji. Hivyo, kinachogawanywa ni asilimia 30 zinazobakia.

Mkataba uliovuja ( TPDC na StatOil hawajaukanusha) unaonyesha kuwa kiwango cha chini kabisa cha uzalishaji Serikali inapata asilimia 30 tu na Mwekezaji asilimia 70 licha ya kwamba tayari gharama zake keshajirudishia. Vile vile kiwango cha juu kabisa cha uzalishaji mgawo unakuwa sawa kwa sawa! Swali la msingi hapa ni, Kwanini makubaliano na kampuni hii ya StatOil yanaenda tofauti na Mkataba elekezi? Je, mikataba yote 26 imekwenda harijojo namna hii? Maswali haya bado hayajajibiwa na TPDC.

Tuelewe

Mkataba wa Gesi Asilia au Mafuta ni makubaliano ya kugawana mapato yanayotokana na kiwango kilichozalishwa. Katika maelezo yao TPDC wanaeleza kuhusu kodi ya mapato, mrahaba na kodi ya huduma. Kodi ya Mapato na kodi ya huduma ni kodi ambazo kila mfanyabiashara nchini anapaswa kulipa. Ikumbukwe kuwa imechukua miaka 20 na kelele nyingi sana mpaka kampuni za Madini kuanza kulipa kodi ya mapato na ushuru wa huduma. Mpaka leo hii bado Halmashauri za Geita na Kahama zinahangaika na kampuni za Madini kulipwa ushuru huu. Kampuni za Madini na za Mafuta hutumia mikakati ya kupanga kukwepa kodi (tax planning measures) kwa kutumia Tax Havens na Mikataba ya Double Taxation Treaties. Hivyo TPDC kusema tutegemee kodi ya Mapato ni sawa na kuimba kama kasuku na baada ya miaka 20 tutajikuta kwenye lawama zile zile za sekta ya Madini. Kwenye baadhi ya mikataba, kodi wanayolipa wawekezaji hukatwa kwenye mgawo wa TPDC na hivyo kodi hiyo hulipwa na TPDC na sio Mwekezaji kama tunavyoaminishwa na Serikali.

Kuhusu mrahaba wa asilimia 5 napo kuna tatizo kwani kwenye mikataba ya Gesi Asilia Mrahaba unalipwa na TPDC maana ndio mwenye leseni na sio Mwekezaji ambaye ni kandarasi tu. Mikataba kadhaa imeandikwa kwa namna ambayo Mwekezaji akilipa mrahaba, anajirudishia kwenye mapato ya Gesi kama gharama. Hivyo kimsingi mapato yetu ya uhakika ni kwenye mgawo wa uzalishaji. Ndio maana tunapiga kelele kuhusu mkataba huu wa StatOil kwenda kinyume na Mkataba mwelekezi wa Serikali.

Tutaambulia kiduchu sana

Kwa kuchambua Mkataba huu kati ya Tanzania na StatOil ya Norway hesabu zinaonyesha kuwa Nchi yetu itapata mgawo kiduchu sana. Chukulia uniti 1000 za gesi asilimia zimezalishwa kwa siku. Uniti 700 zinachukuliwa na Mwekezaji kufidia gharama za kuzalisha gesi hiyo na Uniti 300 zinazobakia Mwekezaji anachukua uniti 150 kama mgawo wake wa faida (profit gas). Hivyo Tanzania itabakia na uniti 150 tu kama mgawo wake, sawa na 15% tu ya Gesi Asilia yote iliyozalishwa katika siku hiyo. Iwapo Mkataba elekezi ungefuatwa Tanzania ingebakia na uniti 240 sawa na 24% ya gesi asilia iliyozalishwa.

Natoa rai kwa vyombo vya habari nchini kuandika masuala haya bila kuyumba maana yanahusu utajiri wa nchi yetu. Dhahabu imebakia mashimo kwa sababu Tanzania ililala na watawala kuandika mikataba ya hovyo. Tusilale kwenye Gesi Asilia. Wakati wa kutaka mikataba kuwa wazi ni sasa. Huu mmoja tu wa StatOil tunaweza kupoteza shilingi 1.6 trilioni, hiyo mingine 26 je? Nchi itabakia kweli? Tusikubali majibu mepesi. Tutake mikataba iwekwe wazi. Uwazi huleta uwajibikaji.

Zitto Kabwe, Mb

17 Julai, 2014

 

Mkataba wa Gesi umevuja: #Tanzania kupoteza shs 1.6 trilioni kwa mwaka – #Norway kujirudishia misaada yake yote nchini kupitia mkataba huu

with 17 comments

Mkataba wa Gesi umevuja: Tanzania kupoteza shs 1.6 trilioni kwa mwaka

-       Norway kujirudishia misaada yake yote nchini kupitia mkataba huu

 Zitto Kabwe, Mb

Mkataba wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji wa Gesi Asilia (PSA) kati ya Shirika la Mafuta na Gesi Tanzania na Kampuni ya Mafuta ya Norway umevujishwa (https://onedrive.live.com/view.aspx?cid=0EC42B180C06D0B8&resid=EC42B180C06D0B8%21107&app=WordPdf). Toka Mkataba huo uvuje na kuanza mijadala kwenye mitandao ya kijamii, habari zake zimekuwa zinazimwa na hivyo kukosa kabisa mjadala mpana kitaifa na hasa kwa wananchi wenye rasilimali zao. Mwanzoni wengi wetu tulidhani (kwa makosa) kuwa tatizo la mkataba huu ni eneo la umiliki wa kampuni tu (shareholding) kulingana na namna ulivyowasilishwa, kumbe mgawanyo mzima wa mapato unakwenda kinyume na maelezo ya Serikali na TPDC kwa umma.

Mkataba uliovuja unaonyesha kwamba makubaliano ambayo Serikali imeingia na Wawekezaji hawa kutoka Norway yanaenda kinyume kabisa na mfano wa mkataba unaotakiwa kusainiwa (Model PSA). Kwa mujibu wa makala iliyoandikwa na jarida la mtandaoni ( http://africanarguments.org/2014/07/04/leaked-agreement-shows-tanzania-may-not-get-a-good-deal-for-gas-by-ben-taylor/ ) Tanzania itapoteza zaidi ya shilingi 1.6 trilioni kila mwaka kulingana na viwango vya uzalishaji wa gesi asilia katika Kitalu namba 2. Kitalu hiki kinamilikiwa na Kampuni ya StatOil ya Norway na kampuni ya ExxonMobil ya Marekani. Norway ni nchi inayosifika duniani kwa kupambana na rushwa na kwa kutumia vizuri rasilimali yake ya mafuta.

Uchambuzi nilioufanya kulingana na viwango vya mgawo wa mapato kati ya ‘model’ PSA na mkataba huu unaonyesha kwamba Tanzania itapata mgawo kiduchu sana na kinyume na mgawo unavyopaswa kuwa. Mgawanyo ni  kama ifuatavyo katika majedwali hapa chini; Ikumbukwe kuwa mgawanyo huu hupatikana baada ya mwekezaji kuondoa gharama zake za uzalishaji, kinachobakia ndio hugawanywa kati ya mwekezaji na Tanzania.

Jedwali 1 Mkataba wa mgawanyo wa Mapato unaopaswa kutumiwa na TPDC (Model PSA) katika Mikataba na Wawekezaji

Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day) Mgawo wa TPDC (Profit Gas)  Mgawo wa Mwekezaji (Profit Gas)
0 249.999 50 50
250 499.999 55 45
500 749.999 60 40
750 999.999 65 35
1000 1249.999 70 30
1250 1499.999 75 25
1500 Above 1500 80 20

 

Jedwali 2 Mkataba wa mgawanyo wa Mapato kati ya TPDC na Statoil/ExxonMobil.

Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day) Mgawo wa TPDC (Profit Gas)  Mgawo wa Mwekezaji (Share of Profit Gas)
0 299.999 30 70
300 599.999 35 65
600 899.999 37.5 62.5
900 119.999 40 60
1200 1499.999 45 55
1500 Above 1500 50 50

 

Ukilinganisha majdwali haya utaona kwamba mgawanyo wa mapato utafaidisha zaidi kampuni ya StatOil na ni kinyume kabisa na mkataba unavyopaswa kuwa.

Wakati mgawo wa nusu kwa nusu upo katika uzalishaji wa chini kabisa kwenye ‘model PSA’, kwenye mkataba wa StatOil mgawo huo upo kwenye uzalishaji wa juu kabisa. Ukilinganisha mgawanyo huu wa mapato, iwapo kiwango cha ‘model PSA’ kingetumika Tanzania ingepata shilingi 1.6 trilioni zaidi ya kiwango itakachopata kwenye mkataba wa sasa uliovujishwa. Hii ni kutokana na Bei ambazo Shirika la Fedha la Kimataifa limeweka katika uchambuzi wake (https://www.imf.org/external/pubs/ft/scr/2014/cr14121.pdf ) kuhusu Gesi asilia ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Mwandishi Ben Taylor katika makala iliyotajwa hapo juu, kiwango cha mapato ambacho Kampuni ya StatOil ya Norway itajipatia kutokana na mkataba huu wa kinyonyaji, katika kipindi cha miaka 15 ya kuzalisha Gesi Asilia nchini itakuwa ni sawa sawa na misaada yote ambayo Tanzania imepata kutoka Norway toka Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961. Tangu Tanzania ipate Uhuru Norway imetoa misaada ya thamani ya $2.5 bilioni, wakati kwa mkataba huu na Kampuni ya StatOil ambayo inamilikiwa na Serikali ya Norway, kwa miaka 15 watapata $5.6 bilioni. Kwa hiyo kwa miaka 7 tu Norway itakuwa imerudisha misaada yote yake mara mbili zaidi!

Kuvuja kwa Mkataba huu kumesaidia sana kuona ukweli wa matamko ya viongozi wetu kuhusu ni namna gani Tanzania itafaidika na utajiri wake wa gesi. Kama kwa mkataba huu mmoja tu Taifa litapoteza matrilioni ya fedha kiasi hiki, ipoje hiyo mikataba mingine 29? Hivi sasa ugunduzi wa Gesi Asilia nchini ni lita za ujazo trilioni 51 ambayo ni sawa na mapipa bilioni 10 ya Mafuta. Katika Gesi Asilia yote iliyopatikana nchini, StatOil peke yao wana jumla ya lita za uzajo trilioni 20, sawa sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4 (zaidi ya mafuta yaliyogunduliwa nchini Uganda na Ghana kwa pamoja). Hata hivyo utajiri wote huu utainufaisha zaidi Norway na Marekani kupitia makampuni yao kuliko watu wa Tanzania. Watanzania watabakia wanapewa misaada ya vyandarua na mataifa haya ilhali wanafaidi Gesi Asilia yetu.

Natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini kutoa tamko kuhusu mkataba huu kati ya Shirika la TPDC na StatOil. Vile vile Kampuni hii ya StatOil kutoka nchi rafiki mkubwa wa Tanzania ina wajibu wa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na mkataba huu. Serikali ieleze ni hatua gani inachukua kurekebisha Mkataba huu. StatOil nao waeleze watachukua hatua gani kuhakikisha wanaacha unyonyaji huu mkubwa na wa aibu kwa Taifa la Norway.

Sasa ni wakati mwafaka Watanzania kuweza kuona mikataba yote ya Gesi na Mafuta ambayo Serikali imeingia na Wawekezaji. Uwazi wa Mikataba sasa. Nimewahi kuandika huko nyuma (http://zittokabwe.wordpress.com/2012/09/17/press-release-contracts-review-is-a-publicity-stunt-and-creation-of-unnecessary-uncertainty-in-the-sector/ ) kwamba njia pekee ya Watanzania kufaidika na utajiri wa rasilimali zao ni kuhimiza uwazi wa Mikataba. Mkataba huu wa StatOil uliovujishwa uwe ni chachu ya kulazimisha Serikali na Makampuni kuweka mikataba yao wazi. Tuanze mashinikizo haya sasa kwa faida ya vizazi vijavyo.

Written by zittokabwe

July 6, 2014 at 11:02 AM

Posted in Uncategorized

Tagged with , ,

Tanzania to lose up to $1b under StatOil PSA: Open these Oil and Gas Contracts

with 8 comments

Tanzania to lose up to $1b under StatOil PSA: Open these Oil and Gas Contracts

ZZK

Zitto Kabwe, MP

When news of the leaked Production Sharing Agreement (PSA) between Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) and Norweigean State Company StatOil came out through social networks, the discussion was muted. When a blogger Ben Taylor wrote a brief about it, some of us saw how serious the issue is. According to the article http://africanarguments.org/2014/07/04/leaked-agreement-shows-tanzania-may-not-get-a-good-deal-for-gas-by-ben-taylor/ Tanzania may be losing up to $1 billion each year depending on the levels of production of natural gas. However, very few people may understand. Took a liberty to simplify the leak and comparing it with the Model PSA which shall be used as a benchmark for these contracts.

Q What exactly is the document?

The leaked document isn’t the PSA per se, but an addendum to the original PSA for Block 2 to take account of the fact that the discoveries are of natural gas, not oil.

The original PSA was agreed with Statoil in 2007 (source, Statoil website). This would have been under Minister Karamagi. The original PSA was presumably based on 2004 Model PSA (pdf). The addendum signed with Statoil was based on the Model PSA Addendum for Natural Gas, finalised in 2008 to take account of contract terms for gas.

The addendum was signed in February 2012, when William Ngeleja was minister.

Q So the leaked PSA is the same as the publicly available model?

For the most part yes, but for the most important part, no. The Model PSA Addendum sets out the following profit gas sharing ratios as seen in Table 1.

 

Table 1 Model PSA Addendum for Natural Gas suggested terms.

Tranches of daily total

Production rates in each of the Contract Areas (MMscf per Day)

TPDC Share of Profit Gas

 

Contractor Share of Profit Gas
0 249.999 50 50
250 499.999 55 45
500 749.999 60 40
750 999.999 65 35
1000 1249.999 70 30
1250 1499.999 75 25
1500 Above 1500 80 20

 

The actual agreed profit gas sharing terms are quite different, as seen in Table 2.

Table 2 Statoil agreed profit gas sharing terms as per leaked document.

Tranches of daily total

Production rates in each of the Contract Areas (MMscf per Day)

TPDC Share of Profit Gas

 

Contractor Share of Profit Gas
0 299.999 30 70
300 599.999 35 65
600 899.999 37.5 62.5
900 119.999 40 60
1200 1499.999 45 55
1500 Above 1500 50 50

 

Clearly, the agreed terms are much better for Statoil and Exxon than the proposed terms.

Q Any other significant terms in the agreement that differ from the model?

Yes. Article 8.1 (i) sets out the Domestic Market Obligation. Ten percent of production is to be reserved for the domestic market. This figure is not included in the model PSA Addendum. The model states that when the proven accessible reserves are determined, then the parties will agree on how much should go into the Gas Commercialisation Project (i.e. the LNG plant) and how much into the domestic market.

The question that arises from this is, by 2012, were the ‘proven reserves’ determined. If so, how much were they?

We know that BG is seeking to have their 10 percent market obligation reduced to zero. At a meeting with stakeholders late last year, they said it was the biggest issue between them and government.

So, are Statoil / Exxon also seeking to have the 10 percent domestic obligation removed?

Was the figure reasonable in the first place?

Q How does this leak affect the conversation about revenues?

Considerably. The IMF released a projection of revenues from LNG (. One key assumption made by that report is that cost recovery is capped at 70 per cent of production and that sharing is on the basis of a six step model with a lowest government share of 35 percent and a highest of 60 percent.

The 70 percent cost recovery limit is founded in the leaked PSA. However, the sharing ratio is quite different. The Model Addendum proposed a seven step model with government share ranging from 50 to 80 percent.

The actual Statoil / Exxon agreement is a six step model with government share ranging from a low 30 percent to just 50 percent at the highest levels.

This makes us ask the question, where did the IMF get the idea of using a six step model in the range of 35 to 60 percent shares for government, when the model was a seven step model ranging from 50 to 80 and the actual Statoil / Exxon agreement was a six step model, ranging from 30 to 50 for government share?

Q Have any other PSAs in Tanzania or the region been released?

In Tanzania, no PSAs have been released. However, Swala Energy in a prospectus they released last year (very big pdf) set out the substantive terms of the two PSAs they hold in Tanzania and the single PSA they hold in Kenya. This type of disclosure is common for small companies seeking to raise capital on stock markets. In fact, the information released in the Swala prospectus goes beyond what is in the leaked Statoil / Exxon addendum and includes the work programme and obligatory payments such as training levy etc.

In Kenya, the CAMAC PSA has been released to the New York Stock Exchange, again to facilitate raising capital. Typically large firms such Statoil or BG are not obliged by capital markets to release individual PSAs, as their overall business isn’t dependent on any single PSA. But small firms such as Swala or CAMAC are often obliged to do so when going to markets.

Q Is it fair that small firms like Swala have to release the terms of their PSAs but big firms like Statoil and BG do not?

Of course not!

Conclusions

For Tanzania to transform our wealth in natural resources to benefit the entire society, TRANSPARENCY must be a key. Let us make a campaign to make all these contracts in Oil and Gas open.

Written by zittokabwe

July 4, 2014 at 3:50 PM

Posted in Uncategorized

Tagged with , ,

Presentation: How can Parliament develop effective ways of dealing with the media to ensure strong advocacy for coverage of Parliament?

leave a comment »

Notes from a presentation on June 30 2014 at Commonwealth Parliamentary Association, local seminar for all Zambian Members of Parliament (Lusaka).

Download How can Parliament develop effective ways of dealing with the Media to ensure strong advocacy for coverage of Parliament?.

Written by zittokabwe

July 1, 2014 at 12:39 AM

Posted in Uncategorized

MCHANGO WA MAANDISHI WA NDG. KABWE ZUBERI ZITTO, MB KUHUSU BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

with 2 comments

MCHANGO WA MAANDISHI WA NDG. KABWE ZUBERI ZITTO, MB KUHUSU BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

Mheshimiwa Spika, Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu za kuweza kuandika mchango wangu huu mdogo kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali mwaka 2014/15. Kama wengi mnavyofahamu mnamo tarehe 1 Juni mwaka 2014 nilimpoteza mama yangu mzazi na kumsitiri siku iliyofuata tarehe 2 Juni, 2014. Huu ni msiba mkubwa sana kwangu na ndugu zangu wote kwani mama yetu Bi. Shida Salum alikuwa nguzo katika familia. Nafahamu kuwa jamaa na marafiki wa mama pia wamepoteza mtu wao muhimu sana. Napenda kuwashukuru nyote kabisa kwa salamu zenu za pole kwetu. Sina namna ya kuelezea shukrani zangu kwenu kwani Bi Shida kwangu alikuwa zaidi ya mama mzazi, alikuwa rafiki, dada na nguzo. Ninamshukuru Allah kwa kuniwezesha kumwuguza na kumsitiri mama yangu. Hakuna amali kubwa ambayo Mungu amenipa zaidi ya hiyo. Nawashukuru tena nyote kabisa wabunge wenzangu kwa kushirikiana nami kwa namna zozote zile kumwuguza na kumsitiri mama yangu. Mungu atawalipa malipo yanayowastahili kwa amali na vitendo vyenu. Sisi kama familia tutaendelea kumwombea dua mama yetu na kumtolea sadaka ili ahifadhiwe mahala pema.

Mheshimiwa Spika, ningependa niwe nanyi katika mjadala huu muhimu wa kila mwaka wa Taifa letu. Hata hivyo bado Mungu hajaniwezesha nguvu za kusimama na kuzungumza. Pindi nitakapowezeshwa nguvu hizo nitakuwa nanyi kwa kipindi hicho nitakachojaaliwa ili kushiriki katika kazi za kuendeleza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha ndugu Saada Salum kwa kuwasilisha Bajeti yake ya kwanza kabisa kama Waziri wa Fedha wa pili Mwanamke wa nchi yetu. Nampongeza kwa kuchukua hatua kadhaa za kuboresha usimamizi wa fedha za umma na hasa matamko aliyotangaza ya kupambana na misamaha ya kodi ambayo imeongezeka mpaka kufikia asiliamia 3.5 ya Pato la Taifa na asilimia 10 ya Bajeti ya Serikali.  Misamaha ya Kodi mwaka 2012/13 ilifikia tshs 1.5 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 15 ya makusanyo yote ya ndani na ni sawa na takribani fedha zote za kodi ambazo Serikali ilikusanya kama kodi ya mishahara ya Wafanyakazi (PAYE). Hata hivyo, matamko ya Serikali yana mapungufu makubwa sana na ni matamko yale yale yanayorudiwa kila mwaka bila utekelezaji. Kuweka wazi misamaha ya kodi na watu au asasi zilizofaidika na misamaha hiyo ni hatua nzuri lakini haitoshi kama hatua hiyo haitaendana na kufanya ukaguzi wa misamaha hiyo. Kamati ya Bunge ya PAC ilitoa agizo mwaka 2013 la kutaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kukagua misamaha ya kodi kama matumizi mengine yeyote ya Serikali. Ieleweke kwamba misamaha ya kodi ni ruzuku (subsidy), ni fedha ya Serikali ambayo iwapo ingekusanywa ingekaguliwa kwa mujibu wa sheria. Matamko ya Serikali ya kuweka wazi misamaha lazima yaendane na kuifanyia ukaguzi (auditing) na kuweka wazi matokeo ya ukaguzi huo. Vilevile ni lazima sasa katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2014/15 kuweka kipengele cha kuzuia misamaha ya kodi kuzidi asilimia moja ya Pato la Taifa na kurekebisha Sheria ya Ukaguzi ya umma wa mwaka 2008 ili kumpa mamlaka ya kisheria CAG kukagua misamaha ya kodi na kuweka wazi matokeo ya ukaguzi huo kwa umma.

Kodi kwa Wafanyakazi

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha ametangaza nafuu ya kodi kwa wafanyakazi wa kima cha chini kutoka kiwango cha 13% mpaka 12%. Kiwango hiki ni kidogo mno na hakimsaidia mfanyakazi kubakia na fedha kwa ajili ya matumizi yake na pia kwa ajili ya kujiwekea akiba. Ni dhahiri kuwa PAYE ni chanzo kikubwa sana cha mapato ya ndani ya Serikali. Kwa mfano mwaka 2013/14 Serikali ilitarajiwa kukusanya tshs 1.5 trilioni kama PAYE ambapo tshs 1 trilioni kutoka idara ya walipa kodi wakubwa na tshs 500 bilioni kutoka idara ya kodi za ndani. Hata hivyo, utaona kuwa mapato haya ni sawa sawa na kodi inayosamehewa kupitia misamaha ya kodi hivyo iwapo misamaha ya kodi ikipunguzwa mpaka kiasi cha asilimia 1 ya Pato la Taifa, Serikali itakusanya kodi ya kutosha kuzipa pengo la punguzo la kodi kwa wafanya kazi. Vile vile Serikali inapoteza kodi nyingi sana kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni makubwa ya kimataifa yanayowekeza hapa nchini (tax evasion and tax avoidance) kwa kiwango cha asilimia 5 ya Pato la Taifa. Iwapo Serikali itajiunga na mikataba ya kimataifa ya kupambana na ukwepaji kodi na pia kuimarisha kitengo cha kodi za Kimataifa ili kupambana na Multinational Corporations ambao wanatumia njia mbalimbali kuhamisha faida zao nje, kutangaza hasara hapa nchini na kukwepa kodi za thamani ya zaidi ya shilingi trilioni mbili kila mwaka kwa mujibu wa takwimu za Global Financial Integrity. Napendekeza kuwa kiwango cha chini cha kipato (mshahara) kukatwa kodi kiwe shilingi 330,000 na kiwango cha chini cha kodi kiwe asilimia 9 tu.

Mheshimiwa Spika, Kiwango hiki cha kodi pia kinawezekana kwa Serikali kuchukua hatua dhidi ya matumizi mabovu ya Serikali. Kwa mfano, kwa mujibu wa Taarifa ya  Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali mwaka 2013, mfumo wa kukagua utumishi wa umma umegundua kuwa jumla ya wafanya kazi wa Serikali 6500 walikuwa wameajiriwa mara mbili kwa majina yale yale, 2700 mara tatu na kulikuwa na watumishi 2500 waliokuwa wanachukua mishahara miwli mpaka mitatu kila mwezi. Baada ya mfumo wa Lawson kuanzishwa jumla ya wafanyakazi  hewa 14,000 waligundulika katika jumla ya wafanyakazi 478,000 wa Serikali. Hatua ya kuondoa matumizi mabovu kutokana na kulipa mishahara hewa pia inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi nchini. Serikali hutumia wastani wa shilingi bilioni 360 kila mwezi kulipa mishahara ambapo katika hizo shilingi bilioni Kumi kila mwezi zimekuwa zikilipwa kwa watumishi hewa. Nafuu ya kodi kwa wafanyakazi nchini katika sekta zote na hasa wafanyakazi wa kima cha chini kitachochea matumizi binafsi ya bidhaa na huduma na hivyo kuchangamsha uchumi na kuwezesha uwekaji wa akiba nchini. Nashauri ukaguzi zaidi ufanyike katika utumishi wa umma ili kumaliza kabisa tatizo la wafanyakazi hewa nchini.

Mheshimiwa Spika ninapongeza kuanzishwa kwa kodi ya zuio kwa ada kwa Wakurugenzi wa makampuni na Mashirika. Kodi hii itaongeza mapato ya Serikali. Hata hivyo kodi kama hii pia itozwe kwenye posho ambazo viongozi wa kisiasa na watumishi wa Serikali wanalipwa isipokuwa posho ya kujikimu (per diem). Vile vile uamuzi wa kuagiza Wizara, Idara na Wakala za Serikali kukusanya maduhuli kwa kutumia mashine za kielektroniki ni uamuzi muhimu sana ambao utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi. Kamati ya PAC iliagiza jambo hili tangu mwaka 2013 na ninaamini kuwa Polisi wa Usalama barabarani wataanza kutoa ‘traffic notifications’ kwa njia hii; pia Wizara ya Ardhi wataanza kutoa Hati za Ardhi za kielektroniki na kukusanya maduhuli kwa njia hii ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini kwa tozo mbalimbali wanazotoza. Juhudi zote hizi lazima zionekane kwa kupunguza mzigo wa kodi kwa Wafanyakazi ambao kiukweli ni wachache (takribani 1.3 milioni) lakini wanabebeshwa mzigo mkubwa wa kodi kuliko wawekezaji wakubwa.

Mheshimiwa Spika, Tanzania haiwezi kuendelea kuwa nchi ambayo Serikali yake inaendeshwa na fedha za wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wahisani. Ni lazima makampuni makubwa ya uwezekaji nchini yashiriki kuendesha Serikali kwa kulipa kodi stahili na kuondoa kabisa misamaha ambayo haina mahusiano yeyote na ukuaji wa ajira nchini na kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo. Vile vile ni muhimu sana kuongeza juhudi za kukuza ajira ili kuwa na wafanyakazi wengi ambao watapelekea kuongeza mapato ya Serikali badala ya kukamua kundi dogo lililopo hivi sasa. Nchini Kenya kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi (PAYE) ni asilimia 10 tu kwa sababu idadi ya walipaji wa kodi hii wanafikia takribani milioni kumi wakati Tanzania ina wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya kila mwezi milioni 1.3 tu.

Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa inaonesha kuwa Tanzania ina jumla wa mifuko mitano ya Hifadhi ya Jamii yenye wanachama 1.3 milioni pekee. Idadi hii ya wanachama ni 6% ya nguvu kazi ya Tanzania. Hata hivyo nguvu kazi ya nchi haipo kwenye wafanyakazi wa mishahara pekee kwani asilimia takribani 70 ya Watanzania wanaishi vijijini na kujihusisha na sekta ya Kilimo. Kwa kuwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii haijafikia wakulima maana yake Watanzania wengi sana wanaishi ya mashaka kwa sababu hawana Bima ya Afya, hawana mafao mengine ya muda mfupi na wala hawana pensheni. Hali hii ni lazima kuirekebisha kama tunataka Taifa lenye maendeleo. Hifadhi ya Jamii sio suala la pensheni tu bali pia ni suala la uwekezaji wa akiba (savings) na uwekezaji wa ndani (investments).

Mheshimiwa Spika, Kasi ya ukuaji uchumi na uwekezaji (Growth and investment rates) vina mahusiano chanya.Takwimu za Penn World Tables (2002) zinaonyesha kuwa kwa nchi 38 za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara wastani wa ukuaji uchumi ulikuwa  0.6% na wastani wa uwiano wa uwekezaji na ukuaji uchumi ulikuwa  10%. Kwa nchi 9 za Asia (9 Asian ‘miracle’ economies), wastani wa ukuaji uchumi ulikuwa 4.9% na wastani wa uwiano kati ya ukuaji uchumi na uwekezaji ulikuwa 25%. Kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa lolote duniani unahusiana moja kwa moja na utayari wa wananchi wa nchi hizo kuweka akiba na kuwekeza vitega uchumi. Takwimu hizi zinaonyesha dhahiri kwamba ili Afrika ipige hatua ni muhimu sana kuimarisha uwekezaji wa ndani ambao unatokana na kiwango cha uwekaji akiba.

Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wa kasi na haraka hauwezekani bila ya sekta ya fedha iliyokita mizizi. Hata hivyo, kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Umasikini nchini (PHDR 2009) mfumo wa kibenki nchini kwetu hautoi msaada wa kutosha kwa wafanyabiashara ndogondogo na wakulima. Mikopo kwa uwekezaji wa ndani ni midogo sana kiasi kwamba haisaidii kuongeza uzalishaji (productivity) na kuhimiza mabadiliko makubwa ya Uchumi (transformation of the economy). Mikopo mingi inayotolewa na mabenki ni kwa matumizi binafsi ya watu na mikopo mikubwa ni kwa shughuli za uchuuzi (trading) badala ya uzalishaji. Hii inathibitishwa na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2013 ambayo inaonyesha kuwa katika mikopo ya thamani ya tshs 10.3 trilioni, ni asilimia 9 tu iliyokwenda sekta ya kilimo. 11.4% viwanda na 25% ilikwenda kwa wachuuzi. Asilimia 17 ya mikopo ilikwenda kwa watu binafsi kwa ajili ya matumizi binafsi!

Kuna haja kubwa ya kufanya mabadiliko makubwa sana ya kimuundo na kisheria na kisera ili kuhakikisha kuwa uzalishaji kwenye kilimo na uongezaji thamani wa bidhaa za kilimo unapata uhakika wa fedha za mikopo. Benki sio rafiki ya Masikini. Benki sio rafiki ya mkulima mdogo hapa nchini. Lazima kubadilika kifikra na kuachana na mazoea. Ni lazima sasa kuweka vivutio kwa wakulima kuweka akiba ya muda mrefu na kuondoa mwiko wa mkulima kutokuwa na pensheni. Hifadhi ya Jamii kwa Mkulima ni suluhisho la kuongeza akiba nchini, kupanua fursa za uwekezaji wa ndani tena kwenye kuongeza uzalishaji wa Kilimo na kujenga jamii ambayo inahifadhiwa. Hifadhi ya Jamii kwa Mkulima pia itaongeza ushindani dhidi ya mabenki katika soko la mikopo midogo midogo na hivyo kumfaidisha mkulima.

Mheshimiwa Spika, mabilioni ya fedha tunayoona yanamilikiwa na mabenki, mifuko ya hifadhi ya jamii, kampuni za bima na asasi za uwekezaji ni matokeo ya kukusanya viakiba vya mtu mmoja mmoja kutoka kwa mamilioni ya watu. Kazi ya asasi za fedha ni kukusanya mabilioni haya na kuyaelekeza kwenye uwekezaji wa miradi mikubwa ianyofanywa na wafanyabiashara na hata miradi midogo kwa wafanyabiashara wadogo. Katika bara la Afrika, hivi sasa watu masikini wanaweka akiba zao katika vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS). Hii ni hali halisi Tanzania, hali ambayo lazima tuijenge kwani mabenki hayapendi kuendesha akiba ndogondogo za watu masikini. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeanza mafao ya mikopo kwa SACCOS za wanachama wao na hivyo kuweza kukopa kwa lengo la kuendesha maisha yao kwa kuongeza uzalishaji hasa kwenye Kilimo. Wafanyakazi wa Sekta rasmi wametungiwa sheria kwamba ni lazima sehemu ya mishahara yao wakatwe kama akiba ya uzeeni na majanga mengine. Waajiri wao pia hukatwa fedha kuchangia pensheni za wafanyakazi wao. Mkulima hana sheria ya kumlazimisha kuweka akiba (na sio lazima kuwepo kwa sheria hiyo) na pia hana ‘mjomba’ wa kumchangia sehemu ya pensheni yake. Hata hivyo Mkulima anachangia 25% ya Uchumi wa Tanzania (GDP) na pia fedha za kigeni. Mchango wa bidhaa za kilimo kwenye mauzo nje umekuwa mdogo kwa sababu wakulima wananyonywa na mabenki na hawana fursa ya mikopo ya kupanua mashamba yao, kununua pembejeo na kufikia masoko mazuri ya bidhaa zao.

Mheshimiwa Spika, Hali ya Uchumi wa Taifa 2013 inaonesha kuwa 20% ya mapato ya fedha za kigeni nchini yanatoka kwenye bidhaa za kilimo ambacho ni Pamba, Kahawa, Tumbaku, Chai, Korosho, Karafuu na Katani. Mazao haya yanaingiza jumla ya dola za kimarekani 867 milioni. Uchumi wetu hauwezi kuondoa umasikini kwa sababu shughuli zake zimejikita kwenye sekta ya madini ambayo inachangia ajira kiduchu (an enclave) lakini inachangia 40% ya mauzo nje. Uchumi wetu ni egemezi na tegemezi kwa sekta moja tu jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi wa maisha ya wananchi. Ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya Kilimo na hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuondoa umasikini vijijini. Mauzo ya bidhaa za kilimo nje yameshuka kwa kiwango cha asilimia 9, zao la Tumbaku ambalo ndio linaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni dola za marekani 307 milioni (zaidi ya shilingi bilioni 500 za kitanzania), mauzo yake yaliporomoka kwa kiwango cha asilimia 12 kutokana na wakulima kutotumia mbolea kwa sababu ya kukosa mikopo katika mabenki kulikosababishwa na unyonyaji wa zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi. Mauzo ya Pamba yalishuka kwa asilimia 32 kutokana na mgogoro wa bei uliosababishwa na kutokuwepo kwa sera ya kufidia bei kwa wakulima (price stabilisation).

Mheshimiwa Spika, suluhisho la mambo yote haya ni kuingiza wakulima kwenye hifadhi ya jamii ili waweke akiba, wapate mafao ya muda mfupi na mrefu na wapate mikopo kupitia vyama vyao vya ushirika vya kuweka na kukopa(AMCOS). Mabenki hayataendelea tena kunyonya wakulima kwa sababu riba zinazotolewa kwa mikopo ya SACCOS/AMCOS ni nafuu na zinaendana na hali halisi ya wakulima. Kupitia kujiunga kwao katika Hifadhi ya Jamii, Fao la fidia ya bei laweza kuanzishwa ili kuwafidia wakulima pale bei za mazao yao zinaposhuka chini ya gharama zao za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la uchaguzi tumefanya mradi huu na hivi sasa wakulima wa kahawa wa vijiji vya Matyazo, Mkabogo na Rusaba kupitia chama chao cha Ushirika cha RUMAKO ni wanachama wa NSSF na tayari wameanza kufaidika na mafao kama bima ya afya na mikopo yenye riba nafuu. Kufuatia mafanikio ya RUMAKO vyama vingine vya ushirika vinavyounda chama kikuu cha KANYOVU chenye vyama 12 vya msingi wamejiunga na NSSF. Tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa wakulima wote wa kahawa wa mkoa wa Kigoma wanahifadhi ya Jamii kupitia vyama vyao vya ushirika. Shirika la NSSF sasa limeanzisha mpango wa kuandikisha wakulima wengi zaidi nchi nzima kupitia ‘Wakulima scheme’. Katika mpango huu NSSF wameshirikiana na Tume ya Ushirika nchini ambayo kuanzia january, 2014 imepewa jukumu la kudhibiti na kusimamia vyama vya ushirika nchini. Ni hatua ya kupigiwa mfano. Hata hivyo bila vivutio vya serikali wakulima hawatajiunga na hifadhi ya jamii kwa wingi tunaoutaka ili kubadilisha kabisa uchumi wa watu wetu vijijini.

Mheshimiwa Spika, Napendekeza ifuatavyo;

  • Serikali ianzishe mpango wa kuwachangia wakulima wanaojiunga na Hifadhi ya Jamii kwa uwiano wa theluthi ya michango yao. Kwa mfano iwapo mkulima atachangia tshs 20,000 kwa mwezi basi Serikali imchangie tshs 10,000 kwa mwezi kwa sharti kwamba iwapo atajitoa kwenye hifadhi ya jamii huu mchango wa Serikali hataupata lakini iwapo akikaa kwenye hifadhi ya jamii kwa miaka isiyopungua kumi/umri wa kustaafu ataweza kupata michango yote na mafao stahiki kwa mujibu wa sheria kama mfanyakazi wa sekta rasmi.
  • Serikali iachane na mpango wa kuanzisha ‘price stabilisation fund’ na badala yake iweke sera kwamba wakulima waliokwenye Hifadhi ya Jamii moja ya fao watakaolipata ni fao la fidia ya bei ambalo litalipwa kwa namna ambayo wataalamu wa ‘actuarial’ wataona ni endelevu.
  • Serikali kupitia Msimamizi wa Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA) waelekeze kuwa mifuko itenge angalau 40% ya akiba wa wakulima kwenye uwekezaji wa kuendeleza miundombinu ya kilimo, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima kupitia SACCOS/AMCOS

Mheshimiwa Spika, iwapo kwa mfano wakulima milioni moja tu nchini walio kwenye vyama vya Ushirika wakijiunga katika hifadhi ya jamii na kuchangia kiwango cha chini kabisa cha tshs 20,000 kwa mwezi (michango itakayokatwa kulingana na msimu wa kilimo cha zao husika) na serikali kuweka kivutio cha tshs 10,000 katika kila mchango wa mkulima mmoja mmoja katika idadi hiyo, jumla ya Michango itakayokusanywa nitakuwa ni tshs 360 bilioni. Wakulima hawa watapata bima ya afya wao, wenza wao na wategemezi 4 na hivyo bima ya afya kufikia Watanzania milioni 6. Fedha hizi zitatumika kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji katika sekta ya kilimo ikiwemo mikopo ya pembejeo, ujenzi wa miundombinu ya kilimo na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaweza kuwekeza fedha hizi kama hisa kwenye Benki ya Kilimo na kuwezesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo. Hii ndio inaitwa ‘Transformation’.

Mheshimiwa Spika naomba kuwasilisha

Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Kigoma Kaskazini.

Kigoma. Juni 17, 2014.

 

HIFADHI YA JAMII KWA SEKTA ISIYO RASMI[1]

with one comment

HIFADHI YA JAMII KWA SEKTA ISIYO RASMI[1]

Zitto Kabwe[2]

Hifadhi ya Jamii ni sera ya Maendeleo. Ni sera inayolenga kuendeleza Maisha ya Watu na kuhakikisha kuwa Watu wanaofaidika na sera hiyo kutotumbukia kwenye dimbwi la Umasikini. Ni kinga dhidi ya kuporomoka kwa kipato kutokana na kifo, ulemavu au Umri. Wanazuoni wanahusisha Hifadhi ya Jamii na tafsiri ya Maendeleo ambayo inajikita kwenye uwezo (capability) ambapo maendeleo yanahakikishwa hata kama mtu hana uwezo wa kufanya kazi. Kwenye mada iliyowalishwa kuhusu uzoefu wa Ghana tumeona namna sekta ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi hiyo ilivyoasisiwa kwa kuanzia akiba ya lazima mwaka 1960 mpaka mfumo wa pensheni mwaka 2010 kupitia Shirika la Umma lililoundwa mwaka 1972 (Social Security and National Insurance Trust – SSNIT). Tanzania ilianza mfumo wa Akiba ya Wafanyakazi mwaka 1964 kama tulivyoelezwa katika historia ya Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) na kuingia kwenye mfumo wa pensheni mwaka 2001. Nchini Ghana mfumo wa kujiwekea akiba kwa hiari (voluntary scheme) umewekwa kwenye sheria zao mbali mbali. Hata hivyo, wakati asilimia 86 ya nguvu kazi ya Ghana ipo katika sekta isiyo rasmi, ushiriki wa wananchi wa nchi hiyo katika Hifadhi ya Jamii ni mdogo kwa kiwango cha 1.23% ya wanachama wote wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini humo. Kwa kuwa mada ya uzoefu wa Ghana na changamoto zake imezungumzwa tayari, tutaona ni namna gani Tanzania inaweza kupanua wigo wa Hifadhi ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa wananchi wengi Zaidi wanafikiwa.

Katika kipindi cha miongo miwili sasa maendeleo makubwa yamefanyika katika sekta ya Hifadhi ya Jamii nchin katika sera na sheria. Hifadhi ya Jamii imetoka mifuko ya Akiba mpaka mifuko ya Pensheni. Hata hivyo kama ilivyo kwa Ghana bado Hifadhi ya Jamii kwa Tanzania ni uwanja wa Wafanyakazi wa sekta rasmi, waajiriwa wa serikali, mashirika ya umma na makampuni binafsi. Watanzania wengi waliojiajiri na walio katika sekta isiyo rasmi hawamo katika mfumo wa Hifadhi ya Jamii. Takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa Watanzania wengi wapo kwenye sekta isiyo rasmi. Takribani asilimia 70 wapo kwenye ukulima mdogo mdogo (vibaku kwa lugha ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi) na wengine asilimia 10 wamejiajiri kwenye shughuli mbalimbali kama biashara ndogondogo, madini, Sanaa, michezo na uchuuzi mwingine. Watanzania wenye ajira rasmi ni sehemu ndogo sana ya nguvu kazi ya Tanzania. Ni dhahiri kuwa Hifadhi ya Jamii Tanzania inawahusu watu kiduchu sana, takribani asilimia 6 tu ya nguvu kazi ya nchi na asilimia 3 tu ya Watanzania wote. Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2013 inaonyesha kuwa wanachama wa mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii nchini ni takribani 1.1 milioni.

Hili ni janga la Taifa. Rundo kubwa la wananchi hawachangii katika kapu la pensheni hivi sasa, hii maana yake ni kwamba huu ni mzigo mkubwa sana na usiokwepeka kwa Taifa pindi idadi ya wazee itakavyoongezeka katika kipindi cha miaka michache ijayo. Tusifumbwe na muundo wetu wa idadi ya watu hivi sasa ambapo Zaidi ya nusu ya Watanzania wana umri chini ya miaka 18 na asilimia 72 wana umri chini ya miaka 30. Hili kundi la watoto linaweza kuwa gawio (demographic dividend) iwapo tutajipanga vizuri. Tusipojipanga hili ni bomu ambalo likilipuka tutatafutana. Ipo siku itafika ambapo hili kundi la watoto halitakuwa na uwezo wa kufanya kazi tena lakini itabidi livishwe na kulishwa. Viongozi wenye maono mapana ya nchi lazima wawe na matayarisho katika masuala kama haya ya nchi. Majawabu yapo nayo ni kuhakikisha kuwa Hifadhi ya Jamii inahusisha watu wengi Zaidi kwa kuandikisha watu katika sekta isiyo rasmi na hasa wakulima na wafugaji, wavuvi na wachimbaji madini, wafanya biashara ndogondogo na wengineo. Huko ndipo pa kuelekea kama kweli tunataka kuwa na Tanzaia imara, bora na yenye neema. Hata hivyo suala hili linahitaji utashi wa kisiasa na maamuzi.

Kuna watu wanaweza kudhani kuwa jambo hili ni ndoto za alinacha. Linawezekana sio tu kwa sekta isiyo rasmi bali kila mwananchi mwenye uwezo wa kufanya kazi ataona umuhimu wa Hifadhi ya Jamii. Hata kwa nchi kama Tanzania jambo hili linawezekana. Kuna mifano kadhaa ya nchi ambazo zimefanikiwa katika jambo hili na kupiga hatua kubwa. Nchi hizi ni kama vile Korea ya Kusini, Thailand na China. Nchi ya China imepata mafanikio makubwa sana kwa kufikisha hifadhi ya jamii kwa wakulima vijijini. Serikali za nchi hizo zimeshikiriana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuhakikisha raia wao wengi wanapata ulinzi wa kijamii ili kupambana na umasikini.

Mkutano na Wakulima wa Kahawa

Mkutano na Wakulima wa Kahawa

Hapa Tanzania tumejaribu katika Mkoa wa Kigoma, Jimbo la Kigoma Kaskazini ambapo wakulima 750 wa Kahawa kupitia chama cha Ushirika cha Msingi kinachoitwa RUMAKO walijiunga na NSSF mwaka 2013 mwezi Machi. Katika mkutano huu tulishuhudia Mwenyekiti wa Ushirika huo Mzee Yahaya Mahwisa akitoa ushuhuda mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Kikwete namna RUMAKO ilivyofaidika baada ya kujiunga na hifadhi ya jamii. Hivi sasa wakulima hawa wana bima ya afya kupitia mpango wa SHIB wa NSSF, wanapata mikopo ya riba nafuu ili kununua Kahawa kwa ajili ya kuuza kwenye mnada na mikopo ya kuboresha mashamba yao na kuongeza ubora wa kahawa na hivyo mapato yao. Kutokana na mafanikio makubwa ya ya RUMAKO vyama vingine 11 vya Ushirika vya Msingi vimejiunga na NSSF katika mkoa wa Kigoma. Vilevile tumeshuhudia Shirika la NSSF likiingia makubaliano ya kikazi na Tume ya Ushirika nchini ambapo Zaidi ya wakulima 400,000 wataandikishwa kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Vile vile tumeshuhudia wachimbaji wadogo wadogo wa madini wakijiunga na Hifadhi ya Jamii. Hatua zote hizi zinatokana na ukweli kwamba RUMAKO imewafungua macho NSSF na sasa inapasa kufungua macho mifuko mingine yote nchini na Serikali ili kufanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini Tanzania.

Sekta ya Kilimo na Sekta ya Madini ni mwanzo mzuri kwa sababu licha ya kwamba ni sekta zisizo rasmi lakini pia ni sekta zenye historia ya kuwa na vyama vya ushirika. Kwa kuwa itakuwa ni changamoto kubwa sana kuandikisha mwanachama mmoja mmoja kwani utawala wake utakuwa mgumu sana, kuandikisha kupitia vyama vya ushirika kutasaidia kuondoa changamoto hizo. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ikiwafikia wakulima ni kama imelifikia Taifa zima maana wao ndio wengi na kwa kweli wakiwa na taarifa za kutosha watafurahia mipango hii. Hata hivyo maeneo mengine kama michezo yanaweza kuwa rahisi kuandikisha kwa Serikali kuweka kanuni kwamba mikataba ya wachezaji na Timu zao ni lazima iwe na kipengele cha Hifadhi ya Jamii. Hii itaondoa kabisa tatizo kubwa la wachezaji wetu hasa wa soka kuishi maisha hohe hahe baada ya kustaafu. Upande wa Sanaa pia na hasa kwa wanamuziki jambo hili linaweza kutekelezwa. Muhimu ni ni kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii kufikisha ujumbe huu kwa wananchi na Serikali kuweka vivutio kwa watu kuweka akiba.

Msingi wa ukuaji wa uchumi wa nchi ni akiba. Uwekezaji wa ndani unahusiana kabisa na uwekaji akiba wa nchi, ndio nadharia za uchumi zinasema. Nchi haiwezi kutegemea tu uwekaji kutoka nje kwani uhuru wa nchi unakuwa hatarini. Nchi zilizoendelea zinaita mitaji kutoka nje kwa sababu tayari mitaji ya ndani imezidiwa. Sisi Tanzania mitaji ya ndani wala hatuna mipango nayo. Hivyo Serikali yeyote makini ni lazima ihamasishe wananchi wake kuweka akiba ili kutumia akiba hiyo kuongeza uzalishaji wa ndani na kuondoa umasikini. Hifadhi ya Jamii ni jawabu la kukuza utamaduni wa kuweka akiba na kutumia akiba hiyo kuwekeza katika sekta zinazokuza ajira na kuchochea uchumi kukua. Kwa wakulima, mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaweza;

-  Kuandikisha kwenye Hifadhi ya Jamii wakulima ambapo watakuwa wamehamasishwa kujiunga kupitia vyama vya msingi vya ushirika. Vivo hivyo hili linawezekana kwa wafugaji na wavuvi. Wachimbaji wadogo wadogo wa madini na pia wafanyabiashara wadogo kupitia vyama vyao wanaweza kuandikishwa pia.

-   Michango kwenye mifuko ambapo wakulima watachangia kulingana na kipato chao kwa kuweka kiwango cha chini kabisa cha mfanyakazi. Kwa kuwa mapato ya wakulima ni ya msimu mifuko itaweka mfumo ambao wakulima watachangia baada ya mavuno yao mara moja. Hata hivyo, kivutio cha Serikali kinatakiwa ili mfumo huu kufikia watu wengi Zaidi. Kwa mfano kama kima cha chini ni shs 20,000 kwa mwezi, basi Serikali itachangia shilingi 10,000 na Mkulima tshs 10,000. Hili linawezekana pia kwa wafugaji, wavuvi na hata wafanyabiashara ndogo ndogo. Iwapo Serikali itaweka kivutio hiki, utamaduni wa kuweka akiba nchini utaongezeka sana na Taifa linaweza kutumia sehemu ya akiba hiyo kufanya uwekezaji katika maeneo yatakayokuza tija kwenye kilimo, kwa mfano uwekezaji kwenye viwanda vya mbolea, viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao na hata mikopo kwa wakulima yenye kuwaongezea kipato na hata kuboresha mashamba yao.

-    Mafao ya wakulima aghalabu hayawi sawa na mafao ya wafanyakazi. Baadhi ya mafao kama Bima ya Afya yatafaidisha wakulima na wafanyakazi. Kwa mfumo wa sasa iwapo Wakulima milioni moja tu watajiunga na Hifadhi ya Jamii, watanzania milioni sita watakuwa wamefadika na Bima ya Afya. Hayo ni mapinduzi makubwa. Taifa linataka nini Zaidi ya kuwa na watu wenye afya? Gharama ya Afya kwa wananchi inaongezeka sana na wananchi wengi wakiwa na Hifadhi ya Jamii tutakuwa tumeondoa mzigo huu kwao na hata kwa Serikali.

Wakulima na hata wafugaji wana changamoto zao. Kwa mfano ukame ukitokea wanashindwa kupata mavuno na hivyo kuingia kwenye dimbwi la umasini kwa sababu wanakosa ‘coverage’. Hasara za namna hii sasa zinaonekana kama ni agenda ya kimaendeleo (see World Bank- World Development Report- Risk and Opportunities, Managing Risk for Development, 2014). Ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa wakulima na wafugaji wakiwa na uhakika wa kutoathiriwa na matendo kama ukame nk huwa wanafanya kazi kwa bidii na jamii kupata maendeleo endelevu. Hifadhi ya Jamii ina majawabu kwa masuala haya kwa kuwa na sera zifuatazo:

Bima ya Ukame/Mvua ambapo wakulima wataweza kufidiwa iwapo kukitokea ukame uatakaoharibu mazao yao au mvua kubwa yenye madhara kama hayo. Sehemu ya mchango wa mwanachama kwenye mfuko wa Hifadhi ya Jamii inaweza kuwekwa pembeni kununulia bima hiyo. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii unaweza kuingia makubaliano na makampuni ya Bima kufanya kazi hii. Tunaweza kujifunza Zaidi eneo hili kutoka nchi za Ghana na India ambazo zimeanza skimu za namna hii.

Mfuko wa Bei ambapo wakulima wanaathirika sana na kupanda na kushuka kwa bei za mazao yao. Hivyo fao hili linaweza kuwekwa katika moja ya mafao ambayo wakulima watapata kwa kujiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Katika mfumo wa namna hii wakulima watalima Zaidi kwani wana uhakika kuwa hata bei zikishuka sana kwenye soko la dunia angalau gharama zao za uzalishaji zitarudi kwa kupitia fao hili. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetangaza kuanzisha ‘Stabilization fund’ kuchukua nafasi ya mbolea ya ruzuku baada ya mfumo huo kugubikwa na ufisadi wa kutisha ambapo katika ruzuku za tshs 584 bilioni zilizotolewa kati ya mwaka 2008/2009 na 2012/2013 ni asilimia 40 tu ndio iliwafikia walengwa na asilimia 60 ililiwa na wajanja wachache haswa mawakala wa mbolea na viongozi wa vijiji. Badala ya Serikali kuweka fedha huko ni vema ikubaliane kuchangia katika michango ya wakulima watakaojiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kauchia mifuko kuwa na ‘Fao la Bei’. Ninashauri Wananchi wote kukataa Fedha za umma kupelekwa kwenye miradi ya majaribio ambayo inatufanya kuongeza Deni la Taifa na badala yake tuisukume serikali kuchangia katika Michango ya wakulima (matching) na hivyo kuongeza uwekezaji wa akiba nchini. Mifuko ya Hifadhi ya jamii itasimamia vizuri zaidi ‘price stabilization fund’ kama ‘Fao la Bei’ kuliko Serikali kwa kufanya uwekezaji makini wenye kulipa (good returns) tena kwenye kuboresha miundombinu ya kilimo, uongezaji wa thamani wa mazao yetu na uboreshwaji wa masoko.

Hifadhi ya Jamii kwa sekta isiyo rasmi, na hapa nimeonyesha kwa wakulima, inawezekana. Hifadhi ya Jamii ni suala la kimaendeleo na ni moja ya dawa ya kuondokana na umasikini ambayo hatukuwa tumeitilia maanani. Jambo bora Zaidi kuliko yote ni kuwa suala hili hatuletewi na wazungu bali ni mawazo yetu wenyewe ya kuhakikisha watu wetu wanakuwa na maendeleo na umasikini unaondoshwa. Hifadhi ya Jamii ni kidonge dhidi ya ufukara na ufukarishwaji. Wito kwangu kwa mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ni kuweka skimu za kuwafikia watu walio kwenye sekta isiyo rasmi na kuweka mafao yanayoendana na hali halisi zao. Wito wangu kwa Serikali ni kuweka vivutio kwa wananchi ili waweze kuweka akiba. Mpango wa kuanzisha ‘price stabilization fund’ uliotangazwa na Serikali hivi majuzi Bungeni wakati wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo ubadilishwe na kuwa ‘matching’ ya Serikali kwa wakulima wanaoweka akiba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

Nimalizie mada yangu hii kwa kurudia mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya PAC kwa takribani miaka 3 sasa ( kabla yake POAC), kwamba hakuna haja ya kuwa na mifuko lukuki nchini. Mifuko iunganishwe na kuwa Mfuko 1 utakaohusika na watumishi wa Serikali, Mfuko 1 utakaohusika na wafanyakazi wa sekta binafsi na kwa kuwa tumeanza skimu za sekta isiyo rasmi basi zikikomaa kuwe na mfuko 1 utakaohusika na sekta isiyo rasmi. Tunaweza kwa mfano kuunganisha NSSF na PPF kuwa mfuko mmoja kwa sekta binafsi, LAPF na PSPF kuwa mfuko wa sekta ya umma na GEPF kujikita kwenye sekta isiyo rasmi.

Vile vile nadhani ni vema badala ya mifuko kuendesha Bima zao za Afya basi zikasimu uendeshaji huo kwa Mfuko wa Bima ya Afya kwa kuchangia kile kiasi ambacho wataalamu wa actuarials wanaonesha kinapaswa kutumika kwa gharama za afya. Hii itaondoa tatizo lililopo la wanachama kuchangia mara mbili kwa gharama za Afya.

Asanteni kunisikiliza

[1] Mada iliyowasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) jijini Arusha 13 -15 Mei 2014.

[2] Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mbunge wa Kigoma Kaskazini

 

Written by zittokabwe

May 15, 2014 at 11:23 AM

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.

Join 126,273 other followers